Na Haji Nassor, Pemba
MAHAKAMA ya Mkoa Chake chake, imemuhukumu kifungo cha miaka 60 jela, mshitakiwa Abubakar Mkulu Bakar (28), mkaazi wa Wambaa Mkoani, baada ya kubainika na kosa la kuwabaka watoto wawili mapacha wa kike (13).
Kijana Abuu ametakiwa kutumikia jela kwa muda wa miaka 30 kwa kila mtoto mmoja, baada ya Mahakama hiyo kutosheka na ushahidi uliotolewa na mashahidi sita akiwemo Daktari na watoto wenyewe ambao walibakwa kwa muda wa miaka miwili mfululizo.
Licha ya adhabu hiyo ya kutumikia jela 60, mshtakiwa huyo alitakiwa kulipa fidia ya shilingi laki 200,000 (shilingi laki mbili) kutokana na madhara makubwa aliyowasababishia watoto hao.
Kabla ya mshitakiwa huyo, kupewa adhabu hiyo, upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na mwanasheria wa Serikali Ali Bilali Hassan alisema, kuwa hakuna rikodi ya kosa kama hilo lakini mshtakiwa ana makosa mengine kadhaa Mahakamani hapo.
Bilali alidai kuwa vile vile Mahakama iangalie kosa ambalo mshtakiwa ametiwa nalo hatiani kwamba ni makosa yaliyozoeleka katika jamii hivyo aliomba Mahakama kumpa adhabu kali mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa vijana wengine wenye tabia kama hiyo.
‘’Muheshimiwa Hakimu naiyomba Mahakama yako tukufu kumpa adhabu kali mshtakiwa huyu, ukizingatia jamii inaisema sana Mahakama kutokana na makosa kama haya kwamba hayapatiwi ufumbuzi na kupelekea kuongezeka siku hadi siku ‘’alisema Bilali .
Baada ya hapo, Hakimu Khamis Ramadhan ,alimpa nafasi mshtakiwa, na kuiomba Mahakama imfikirie kwa kumpunguzia adhabu kutokana na kukaa rumande kwa muda mrefu, na kwamba anafamilia inayomtegemea ombi ambalo lilitupwa na Mahkama.
‘’Kama Mahakama imenitia hatiani, Muheshimiwa Hakimu kutokana na tuhuma hizi zidi yangu, naiyomba inionee huruma kwa kunipunguzia idadi ya miaka, ambayo imeniandikia juu ya kosa hili, ambalo lilipangwa juu yangu’’, alidai Abuu.
Awali mshitakiwa Abubakar Mkulu Bakar, alitenda kosa hilo baina ya mwaka 2011 na mwaka 2013 huko Wambaa Mkoani ,Tanga na Mwanza Tanzania baram ambapo ilithibitisha kuwabaka watoto hao kwa pamoja na kuwasababishia maumivu makali katika sehemu zao za siri.
Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu 125 (1) (2) (e) na kifungu 126 (1) sharia namba 6 ya mwaka 2004, sheria ya Zanzibar iliyopitishwa na baraza la wawakilishi Zanzibar , ambapo pia Mahakama hiyo imetoa haki ya rufaa ndani ya siku 30 kukara rufaa kwa yeyote asieridhika na hukumu hiyo.
Hivi karibuni Mahakama hiyo ya Mkoa Chake chake, ilimuhukumu kifungo cha miaka 15 jela, mshitakiwa Issa Ali Mohamed (28), baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kubaka mtoto wa kike (5) na Ali Mohamed Ali (22) mkaazi wa Kwale Miburani, kifungo cha miaka (30) jela, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike (12).
………………………………………………….. MWISHO ……………………………………………………….
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni