Jumamosi, 24 Agosti 2013

Na Haji Nassor, Pemba WAJUMBE wa mpango wa utekelezaji wa TASAF awamu ya tatu kisiwani Pemba, wametakiwa kuwa na ushirikiano wa pamoja, katika kusimamia mpango wa kuzinusuru kaya masikini kwa kuzijengea ufahamu ili zishiriki vyema katika utekelezaji wa miradi. Hayo, yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi alipokua akifunga warsha ya siku mbili, iliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha mafunzo ya amali Vitongoji, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba. Alisema kuwa, lengo kuu la warsha hiyo, ilikuwa ni kukuza uwelewa kwa wadau wote, ambao wanatakiwa kusimamia mpango wa utekelezaji na kuhakikisha kila mwenye vigezo anafaidika katika miradi hiyo. Alisema katika utelezaji wa TASAF kwa amu hii ya tatu mpya, itatekelezwa katika shehia kwa kuzifikia kaya masikini zaidi moja kwa moja, kwa kuzijengea uwezo wa kujiwekea hakiba ambazo zitawasaidia kwa kujipatia maendeleo na kuondokana na umasikini. ‘’Mimi naamini kama sisi viongozi kuanzia ngazi ya shehia ha Mkoa tukijipanga vyema, basi kaya ambazo ni maskini zinaweza kufanikiwa kupubnguza joto walilonalo’’,alisema Mkuu huyo wa Mkoa. Kabla ya ufungaji wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania TASAF, Ladis Slaus Mwamanga, alisema, mfuko huo kwa awamu ya tatu, umejipanga vyema ili kuhakikisha kila mlengwa anafikiwa. ‘’TASAF ina kawaida ya kufanikiwa katika awamu zote, hivyo tumeona ni vyema kueleweshana yale mapya, ambayo yanapaswa kujilikana na wote, na kila mapungufu yaweze kuelezwa na kuyafanyia uchambuzi yasiweze kutokea tena'', alisema Mkurugenzi huyo. Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tidwa aliwataka watendaji kushiriki kikamilifu pamoja na kuchangia katika nafasi zao, kuweza kufanikisha malengo ya awamu ya tatu ya TASAF ya kuwaondolea wananchi umaskini. “Natarajia kila mmoja wetu ,atatekeleza vyema majukumu yake kwa wananchi, ambapo wajumbe wa sheha mutakuwa na kazi kubwa ,katika majukumu mbali mbali hivyo naomba muwe makini'', alisisitiza Mkuu wa Mkoa. Kwa upande wake ,Afisa Mdhamin Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Pemba,Amran Masoud Amran, alieleza mpango wa TASAF awamu ya tatu ni kuzisaidia nguvu za wananchi pamoja na kupambana na umasikini kwa kuwapatia wananchi huduma muhimu za msingi. Akitoa mada katika warsha hiyo, muwezeshaji Amadeus Kamagenge, alisema, mpango wa kuziwezesha kaya masikini ,ni kuwaongezea kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu ya wananchi ,ambayo yatafikiwa baada ya utekelezaji. Katika TASAF awamu iliyopita kisiwa cha Pemba, kilibahatika kupata miradi 366 ya aina mbali mbali ikiwa ni pamoja na uvuvi iliyogharimu zaidi ya shilingi 6 bilion na 22 milion. MWISHO.

wajumbe wa Kamati Tendaji wakiwa kwenye picha ya pamoja huko Chake chake Pemba, mara baada ya kumaliza mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji hao, kwenye awamu ya tatu ya utekelezaji wa TASAF, akiwa na wakuu wa Wilaya na Mikoa ya Pemba (picha na Haji Nassor, Pemba)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni